Milipuko mipya imetokea hivi pude siku ya Jumatano Septemba 18 katika viunga vya kusini mwa Beirut, na pia kusini na mashariki mwa Lebanon. Milipuko ya hivi punde pia inahusisha vifaa vya mawasiliano vinavyotumiwa na Hezbollah, chanzo cha usalama kimeliambia shirika la habari la Reuters., pamoja na vifaa vingine vya mawasiliano ya simu. Duka la simu za rununu pia zimeathirika. Kwa mujibu wa serikali ya Lebanon, takriban watu 20 waliuawa na wengine zaidi ya 450 kujeruhiwa.
Milipuko ya vifaa vya mawasiliano inaendelea kuripotiwa nchini Lebanon. Takriban watu 20 wameuawa siku ya Jumatano Septemba 18 katika milipuko mipya ya vifaa vya mawasiliano, imetangaza Wizara ya Afya ya Lebanon, pia ikiripoti zaidi ya watu 450 kujeruhiwa. Walkie-talkies, simu za rununu na njia zingine za mawasiliano zimeripotiwa kutumika kama vilipuzi, ambazo baadhi zililipuka wakati wa maandamano ya mazishi ya wahanga wa milipuko ya siku iliyotangulia.
Hali ya taharuki imeendelea kushuhudiwa katika kitongoji cha Dahiya, kusini mwa mji wa Beirut na ngome ya Hezbollah.
Katika vitongoji vya kusini mwa Beirut, magari mengi ya kubebea wagonjwa na magari ya zimamoto yaliingia barabarani, yakiacha hofu na uharaka, anaripoti mwandishi wetu huko Beirut, Sophie Guignon, ambaye alikuwa katika ngome hii ya Hezbollah wakati wa milipuko. Wakati huo huo, mazishi yalifanyika kwa watu wanne, ikiwa ni pamoja na mtoto wa naibu wa Hezbollah, aliyeuawa siku ya Jumanne katika milipuko ya kwanza ya mawasliano.
Bado haijafahamika ni vifaa vipi vilivyoathiriwa na milipuko ya siku ya Jumatano. Inaweza kuwa vifaa vya mawasiliano vinavyotumiwa na jeshi, lakini pia kunaweza kuwa na vifaa vingine kama vile simu au kompyuta.
Hata hivyo, vifaa vinaonekana kuwa vikubwa zaidi kuliko vilipuzi vya siku iliyopita, ikimaanisha kwamba milipuko hiyo ilikuwa na nguvu zaidi: majeraha na uharibifu uliosababishwa na milipuko hii ya hivi punde kwa hiyo ni mbaya zaidi, anaripoti mwandishi wetu huko Beirut, Paul Khalifeh. Aidha, vifaa hivyo havikuwa vinatumiwa na wanachama wa Hezbollah pekee, bali pia na raia.
Hali ya hasira pia ilitanda katika kitongoji hicho, huku ndege isiyo na rubani ya Israel ikiruka juu ya eneo hilo.
Milipuko mingine iliripotiwa huko Saida (Kusini) na Baalbeck (Mashariki), ambapo watu 15 walijeruhiwa, chanzo cha hospitali kiliiambia shirika la habari la AFP. Milipuko ilitokea katika nyumba, ambazo baadhi ziliharibiwa vibaya, ndani ya magari ambayo yalishika moto.
Jeshi la Lebanon liliwataka raia kutokusanyika katika maeneo yaliyoathiriwa na "matukio haya ya usalama" ili kuwezesha uokoaji wa waliojeruhiwa na timu za uokoaji. Mamia ya wachangiaji damu walielekea katika hospitali, ambazo zilipokea karibu watu 3,000 waliojeruhiwa siku moja kabla.
Slovenia ambayo inashikilia zamu ya uweyekiti wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imtangaza mkutano wa dharura siku ya Ijumaa Septemba 20 kuhusu mfululizo wa milipuko mibaya huko Lebanon.