Msemaji wa polisi Resila Onyango amethibitisha tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia leo na kuongeza kuwa wanafunzi wengine 14 wamejeruhiwa vibaya, na wamekimbizwa hospitalini.
Inaelezwa kwamba moto huo ulianza usiku wa kuamkia leo wakati wanafunzi hao wakiwa wamelala kwenye bweni lao.
"Kuna wanafunzi 17 ambao wamethibitishwa kufariki wakati wengine wakiwa wamepelekwa hospitalini wakiwa na majeraha mabaya.” amesema msemaji wa polisi Resila Onyango.
Licha ya kuthibitisha mkasa huo, maofisa wa polisi hawajatoa maelezo kuhusu umri wa waathiriwa wa mkasa huo.
Aidha msemaji huyo wa polisi ameeleza kwamba miili ambayo imeondolewa kwenye eneo la mkasa imechomeka kiasi cha kutotambulika.
Kati ya wanafunzi wengine waliojeruhiwa, 16 kati yao wanaendelea kupokea matibabu wakiwa na majeraha mabaya zaidi kama iliyoeleza taarifa ya polisi.
Inaelezwa kwamba huenda miili zaidi ikapatikana kutoka katika eneo la mkasa.
Hadi tukichapisha ripoti hii, chanzo cha moto huo hakikuwa kimebainika lakini uchunguzi ulikuwa umeanzishwa.
Visa vya moto kwenye shule vimekuwa vikiripotiwa nchini Kenya haswa katika shule za bweni ambapo mwaka wa 2017, wanafunzi 10 waliteketea kwenye moto katika shule ya Moi Girls jijini Nairobi.
Wanafunzi wengine 67 waliteketea katika ajali nyengine ya moto miaka zaidi ya 20 iliopita katika shule moja katika kaunti ya Machakos, Kusini mashairki mwa jiji kuu la Nairobi