Mwanafunzi wa kidato cha Kwanza Afariki baada ya Kuokota Kilipuzi

Familia moja katika eneo bunge la Bumula kaunti ya Bungoma imejawa na majonzi kufuatia kufariki kwa mwanao baada ya kuokota kilipuzi cha kuchimba madini kimakosa.

Mwanafunzi wa Shule ya Upili ya St. Kizito Mayanja anaripotiwa kuchukua kilipuzi kinachodhaniwa kuwa cha mgodi bila kujua Jumanne, Oktoba 8, alipokuwa akitembea nyumbani. Kwa mujibu wa ripoti ya TV47, kijana huyo mwenye umri wa miaka 16 alikichukua kilipuzi hicho cha mgodi nyumbani kwake, ambako baadaye kililipuka.


"Alikuwa tu ndani ya nyumba wakati niliposikia mlipuko. Nilikimbia ndani ya nyumba na kumkuta mwanangu ameumia; vidole vyake vilikuwa vimejeruhiwa, na tumbo lake pia lilikuwa limejeruhiwa.

Alikuwa ameumia kila mahali," alisema mama wa mvulana huyo. Familia hiyo inadai mtoto wao alichukua kifaa hicho cha mlipuko kutoka kwa kampuni ya Kichina inayojihusisha na mgawanyo wa mawe katika eneo hilo. "Tulianza kutafuta chanzo cha mlipuko.

Hapo ndipo tulipokipata kilipuzi cha mgodi kilichomuua mtoto wetu. Nina mabaki yake nyumbani kwangu," alisema jamaa mmoja wa familia hiyo. Wakazi wa eneo hilo wanailaumu kampuni hiyo kwa kutowafahamisha umma kuhusu hatari za kuwa na kampuni hiyo karibu.

"Mtoto huyu hakujua alichokichukua. Kama kampuni ingekuwa imezungusha uzio katika eneo lao na kuweka usalama wa kutosha, nadhani tusingekuwa katika hali hii leo," alisema mkazi mmoja. 

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii