Mafuriko nchini Nepal: idadi ya waliofariki yaongezeka hadi 101 na 64 hawajulikani walipo

Takriban watu 101 wamefariki na wengine 64 hawajulikani walipo nchini Nepal, kufuatia mafuriko na maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua kubwa, hasa katika mji mkuu Kathmandu, kulingana na ripoti mpya iliyotangazwa na polisi siku ya Jumapili.


"Idadi ya waliofariki ni 101 na watu 64 hawajulikani walipo leo asubuhi," msemaji wa polisi Dan Bahadur Karki ameliambia shirika la habar la AFP.

Ripoti ya awali ya polisi ya siku ya Jumamosi iliripoti takriban watu 59 waliofariki na 44 kutoweka. "Inawezekana kwamba idadi ya watu itaongezeka wakati kazi yetu ya utafutaji na uokoaji ikiendelea katika maeneo yaliyoathirika," msemaji wa polisi Dan Bahadur Karki ameliambia shirika la habari la AFP.

"Hii ndiyo mvua kubwa zaidi iliyorekodiwa katika mji mkuu tangu angalau miaka ya 1970"

Bonde la Kathmandu lilirekodi mvua ya milimita 240 kwa muda wa saa 24 kati ya Ijumaa na Jumamosi asubuhi, mamlaka ya hali ya hewa nchini Nepal imeliambia Gazeti la Kathmandu Post. Hii ndiyo mvua kubwa zaidi iliyorekodiwa katika mji mkuu wa Nepal tangu angalau 1970, kulingana na shirika hili.

Mamlaka ilikuwa imeonya kuhusu mafuriko ya ghafla katika mito kadhaa wakati hali mbaya ya hewa ilipoanza. Mito ya Kathmandu ilifurika, ikasababisha mafuriko katika nyumba zilizo karibu na kingo.

Mafuriko ya mara kwa mara zaidi

“Inatisha. Sijawahi kuona uharibifu kama huu,” amesema Mahamad Shabuddin, 34, mmiliki wa ibanda cha kutengeneza pikipiki karibu na Mto Bagmati uliojaa maji Jumamosi. Baadhi ya walionusurika walikimbilia kwenye paa za majengo, wengine walikimbia kupitia maji ya matope.

Monsuni kuanzia Juni hadi Septemba husababisha vifo na uharibifu kote Asia Kusini kila mwaka, lakini idadi ya mafuriko hatari na maporomoko ya ardhi imeongezeka katika miaka ya hivi karibuni.

Zaidi ya watu 220 wamekufa mwaka huu nchini Nepal katika majanga ya asili yanayohusiana na mvua.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii