Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema serikali ipo katika mchakato wa kudhibiti madaktari wanaofanya kazi kwenye hospitali zaidi ya moja na vituo vya afya binafsi.
Hayo ameyasema leo Julai 30,2024 katika kongamano la kumbukizi ya Rais mstaafu wa awamu ya tatu,Hayati Benjamini Mkapa linaloendelea kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere JNICC jijini Dar es salaam.
Amesema zaidi ya madaktari 5000 waliohitimu na kuwa na sifa za kuajiliwa bado wanasota mtaani kwa kukosa ajira rasmi ambapo wanakadiliwa kutumia zaidi ya bilioni 450 kusomea fani hiyo.
“Kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya madaktari vijiweni serikali imeona sasa ipo haja ya kulitafutia ufumbuzi swala hilo sasa itaanza kudhibiti madaktari wote wanaofanya kazi kwenye hospitali zaidi ya moja na vituo vya afya vya binafsi maana hawa ndio wanaowazibia wengine”.Amesema.
Amesema Madaktari wameruhusiwa kuanzisha hospitali zao baada ya muda wa kazi lakini kinachoonekana sasa daktari mmoja anafanyakazi zaidi ya vituo viwili hali hiyo inapelekea kuminya ajira kwa madaktari wengine waliopo mtaani.
“Kama una hospitali tutakupa maelekezo asilimia kadhaa ya unaowaajili wasiwe kwenye ajili ya kudumu na sasa na sasa tupo kwenye uchambuzi na utakapokamilika tutaufikisha kwa waziri mkuu”Amesema Ummy.
Kwa upande wake Mtendaji mkuu wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Dkt Ellen Mkodya-Senkoro amesema kupitia utoaji wa huduma za afya wameweza kuwafikia wananchi zaidi ya milioni 32 ambapo pia wametoa ajira zaidi ya 13,000 kwenye sekta ya afya.