WAKAZI wa eneo la Metameta katika mtaa wa Manyatta Kaunti ya Kisumu Jumatatu waliamkia habari za kushangaza baada ya watoto kuwaeleza majirani jinsi baba yao alivyomuuwa mama yao wakishuhudia na kisha kujitoa uhai.
Hii ilibainika baada ya majirani kuwaona watoto hao wakicheza nje asubuhi bila kuwaona wazazi wao, jambo ambalo halikuwa kawaida yao.
Awali, mhudumu wa bodaboda ambaye huwapeleka watoto hao shuleni alifika kuwachukua lakini akaondoka mara baada ya kifungua mimba mwenye umri wa miaka 6 kumwambia kuwa, ‘watu wamekufa hapa ndani.’ Alifikiri mvulana huyo anatania, hivyo akaondoka.
Mtu aliyefuata kuwauliza watoto hao kuhusu wazazi wao ni landledi, Margaret Otieno.
“Nilikuwa nimeanza kufua nguo nje ya nyumba yangu nilipoona watoto wanacheza, nikataka kujua kwanini hawaendi shuleni na wazazi wao waliko, waliniambia kuwa wazazi wao wamefariki. Nilidhani wanacheza hadi nilipoingia ndani ya nyumba yao,” alisema Bi Otieno.
Alipomwona baba wa watoto hao akiwa amelala sakafuni, Bi Otieno alitoka mbio na kuelekea moja kwa moja hadi nyumbani kwa jirani yake ambaye ni daktari aliyetambulika kama Bw George Omondi.
“Mwanaume huyo alikuwa amelala chini, sikutaka kumgusa hivyo nikammulika na tochi yangu na kugundua kuwa macho yake yalikuwa yametulia, hayapepesi, alionekana kutokwa na povu mdomoni pia,”
“Sikujua kuwa mkewe marehemu pia alikuwa ndani ya nyumba hadi nilipouona mwili wake kitandani ukiwa umejaa damu huku kisu kikiwa karibu naye,” akasimulia Bw Omondi.
Kwa kutaka kujua kilichojiri katika nyumba hiyo, Bw Omondi na Bi Otieno waliamua kuzungumza na watoto hao.
Kifungua mimba wao aliwasimulia jinsi alivyomuona baba yake akimshika mama yao mdomoni na kumchoma kisu mara kadhaa.
Kijana huyo pia aliwasimulia majirani waliokuwa wamechanganyikiwa jinsi alivyomwona babake akijaribu kujinyonga kwa kamba lakini akashindwa na hatimaye kuanza kunywa sumu.
Kulingana na ripoti ya polisi iliyowasilishwa katika Kituo cha Polisi cha Kondele wawili hao hawakuwa na mvutano wa kinyumbani hivyo ikafanya hata majirani kukosa kusikia yaliyotendeka.
Ripoti ya polisi ilisema zaidi kwamba mwanamume huyo aliyetambuliwa kama Felix Owiti, 32, alionekana akiwa na hasira kazini siku ya Jumapili.
“Mwajiri wa mwathiriwa, mmiliki wa baa, alibainisha kuwa marehemu alikuwa na hasira usio wa kawaida akiwa kazini na hata kumwitisha mwajiri wake pesa ambazo zinaaminiwa alitumia kununua sumu,” ilisema taarifa hiyo ya polisi.