Tume ya kitaifa ya haki za binadamu nchini Kenya, imesema idadi ya watu waliokufa kutokana na maandamano yaliyoanza mwezi uliopita imefikia 50 baada ya hapo jana watu wawili kuripotiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi katika maandamano mapya ya kutaka rais William Ruto, aachie ngazi.
Karibu siku nzima, polisi walitumia mabomu ya machozi kuwasabaratisha waandamanaji, waliokusanyika katikati ya jiji la Nairobi.
Waandamanaji hawa wanaeleza ni kwanini wamejitokeza.
“Niko hapa kama mwanafunzi wa chuo kikuu kuandamana kutaka kufahamu ni kwa nini ufadhili wa wanafunzi wa vyuo vikuu uliondolewa.” Alisema mmoja wa waandamanaji.
Shughuli nyingi kama vile usafiri zilionekana kukwama huku maduka vile vile afisi za serikali zikisalia kufungwa.
Maandamano haya yalianza mwezi mmoja, uliopita yakiongozwa na vijana maarufu kwa jina la Jenzi, na kusababisha rais Ruto kuachana na mswada wa fedha na hata kulifuta baraza la Mawaziri.
Lakini, je, waandamanaji wanataka nini zaidi?
“Uamuzi ambao rais alifanya wiki iliopita ulikuwa mzuri sana ila kuna mambo mengi sana anayostahili kuyatekeleza.” Alismea mwanadamanaji mwengine.
Maandamano haya yamefanyika huku Tume ya taifa ya kutetea haki za binadamu katika ripoti yake siku ya Jumanne ikisema watu 50 wamepoteza maisha na wengine zaidi ya 400 wamejeruhiwa baada ya polisi kutuhumiwa kuwapiga risasi wakati wa maandamano yaliyopita.