Makamu wa rais wa Marekani na mgombea wa urais wa chama cha Democratic Kamala Harris na rais wa zamani wa Marekani na mgombea wa chama cha Republican Donald Trump wamekubali kufanya mdahalo Septemba 10 utakao andaliwa na shirika la Marekani la ABC News.
Kamala Harris na Donald Trump, wagombea wa uchaguzi wa urais wa Marekani, watafanya mdahalo Septemba 10 kwenye kituo cha televisheni cha ABC, kituo hicho kimethibitisha hivi punde siku ya Alhamisi.
"Makamu wa Rais Harris na rais wa zamani Trump wote wamethibitisha kuwa watashiriki katika mdahalo wa ABC," kituo hicho kimesema.
Shirika hilo lilithibitisha mpambano huo katika chapisho kwenye X, zamani ukiitwa Twitter, baada ya Trump kusema Alhamisi kwamba atakuwa tayari kufanya mdahalo na mpinzani wake wa chama cha Democratic mara nyingi kabla ya uchaguzi wa Novemba.
Wakati huo huo Donald Trump amesema itakuwa vema wawili hao wafanye midahalo mitatu.
"Tunafikiri tunapaswa kufanya midahalo mitatu," Trump alisema, akipendekeza midahalo miwili ya ziada ambayo alisema itaandaliwa na Fox News na NBC.
Naye Bi Harris amesema yuko tayari kushiriki midahalo ta ziada lakini akasema kwana yuko tayari kuhudhuria mdahalo wa ABC akiwa kwenye hafla katika jimbo la Michigan siku ya Alhamisi.
ABC News ilisema kuwa mdahalo huo utasimamiwa na mtangazaji mkuu wa kipindi cha World News Tonight David Muir na mtangazaji mkuu wa ABC News Live Linsey Davis.