Jeshi la Polisi nchini Tanzania limesema uchunguzi kuhusu tukio la udhalilishaji kwa binti mmoja Jijini Dar es salaam unaendelea vizuri huku likisema kuwa watu wenye taarifa za ziada waziwasilishe kwa njia sahihi kwa kutumia mifumo iliyopo bila kuendelea kumuumiza msichana huyo.
Taarifa ya Jeshi la Polisi imeeleza kuwa watu waendelee kutafakari namna wanavyoendelea kujadili jambo hilo na kutoa maoni kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari na kujiuliza kama kufanya hivyo sio kuendelea kumtonesha majeraha ya moyoni aliyonayo binti huyo na familia yake
"Jeshi la Polisi lingependa kueleza kuwa uchunguzi unaendelea vizuri na wananchi waendelee kuwa na subira kwani taarifa itatolewa baada ya kukamilisha yale ambayo sheria za nchi zinavyioelekeza" imesema taarifa hiyo.