Mamia ya watu waliandamana mjini Tunis siku ya Jumapili kumuunga mkono Rais Kais Saied huku kukiwa na ukosoaji mkubwa ndani na nje ya nchi baada ya wimbi la kukamatwa kwa waandishi wa habari, wanaharakati na mawakili.
Umoja wa Ulaya, Ufaransa na Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu walielezea wasiwasi wao kutokana na kukamatwa kwa watu hao katika msako uliofanywa na polisi kwenye makao makuu ya chama cha wanasheria mwezi huu ambapo mawakili wawili wanaomkosoa rais walitiwa ndani.
Polisi mwezi huu iliwakamata watu 10, wakiwemo waandishi wa habari, wanasheria na maafisa wa mashirika ya kiraia, katika kile kilichoelezewa na Amnesty International na Human Rights Watch, kuwa msako mkali sana, ambao uliitaka Tunisia kuheshimu uhuru wa kujieleza na uhuru wa kiraia.
Wiki iliyopita, mawakili waligoma, wakisema mmoja wa mawakili wawili waliokamatwa katika uvamizi uliofanywa katika chama cha wanasheria aliteswa, madai ambayo yamekanushwa na Wizara ya Mambo ya Ndani.