Mwandamanaji mmoja amefariki baada ya kupigwa risasi na polisi

Nchini Kenya, mtu mmoja amethibitishwa kufariki katika maandamano yaliofanyika Alhamis ya wiki hii jijini Nairobi kupinga muswada mpya wa fedha mwa mwaka wa 2024.

Kwa mujibu wa shirika la kimataifa la kuetetea haki za binadamu la Amnesty International, raia huyo alifariki baada ya kupigwa risasi na afisa wa polisi.

Maandamano hayo yalioongozwa kwa sehemu kubwa na vijana, yalianza jijini Nairobi mapema wiki hii kabla ya kusambaa katika miji mingine kupinga mapendekezo ya serikali ya Rais William Ruto kuongeza ushuru katika bidhaa mbalimbali kupitia muswada huo wa fedha.

Vijana hao wanasema wamechoshwa na sera za Rais William Ruto kuhusu uchumi haswa wakati huu ambapo idadi kubwa ya raia katika taifa hilo la Afrika Mashariki wanakabiliwa na ugumu wa maisha.

Licha ya maandamano hayo ya Alhamis kuwa yenye utulivu, maofisa wa polisi waliwarushia waandamanaji mabomu ya machozi na maji ya kuwasha wakijaribu kuwazuia kuelekea katika majengo ya bunge.

Kwa mujibu wa mamlaka huru ya kuangazia utendakazi wa polisi nchini kenya IPOA, wamepokea taarifa ya kufariki kwa mwandamanaji na wameanzisha uchunguzi.

Taarifa ya polisi inasema mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 29 alifariki baada ya kuwasili katika hospitali moja jijini Nairobi akiwa na majeraha bila ya kutoa maelezo zaidi.

Mathias Kinyoda, msemaji wa Amnesty International Kenya, amesema mwandamanaji huyo alipigwa risasi wakati akijaribu kuwatoroka polisi waliokuwa wakiwakabili waandamanaji.

Aidha ameeleza kwamba, mwanaume huyo alipigiwa risasi na afisa wa polisi ambaye hakuwa amevalia sare rasimi za kazi na kutaka uchunguzi kufanyika.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii