Chama cha Gnassingbe cha Union for the Republic Party (UNIR) kilipata viti 108 kati ya 113 katika uchaguzi uliofanyika Jumatatu iliyopita, kulingana na matokeo ya muda yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi Jumamosi.
Idadi ya wapiga kura ilikuwa asilimia 61, kulingana na takwimu za tume ya uchaguzi, lakini ushindi ni kamili kwa Gnassingbe, aliye madarakani tangu mwaka 2005 baada ya baba yake Gnassingbe Eyadema aliyetawala taifa hilo dogo la Afrika Magharibi kwa karibu miongo minne.
Kwa mujibu wa katiba mpya iliyoidhinishwa na wabunge mwezi Aprili, Gnassingbe ataweza kuchukua wadhifa mpya kama rais wa baraza la mawaziri, jukumu linalofanana na la waziri mkuu, ambalo linachukuliwa moja kwa moja na kiongozi wa chama chenye wabunge wengi.
Vyama vya upinzani vilikosoa mabadiliko ya katiba na kuyataja kuwa “mapinduzi ya kitaasisi”, na kuunda jukumu lililowekwa makusudi kumnufaisha Gnassingbe kukwepa ukomo wa mihula ya rais na kuimarisha utawala wa familia yake.