Dereva Ajali iliyoua Watoto Arusha Apandishwa Kizimbani

Dereva Luqman Hemed Juma Mkazi wa kata ya Sinoni Mkoani Arusha aliyekuwa akiendesha Basi la Shule ya Ghati Memorial ( Toyota Hiace) lililopata ajali na kuua Wanafunzi nane April 12 2024, amekamatwa na kufikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha April 16 na kusomewa mashtaka nane ya kuua bila kukusudia.


Wakisoma mashtaka hayo, Waendesha mashtaka wa serikali Yunis Makala na Amina Kiango wamesema Mshtakiwa huyo akiwa dereva akiendesha gari T496EFK Toyota hiace April 12 2024 bila kuchukua tahadhari na kuzingatia usalama wa Abiria aliowabeba waliokuwa chini ya uangalizi wake, aliliendesha gari hilo kwenye maji ya mvua eneo la Engosengiu, Sinoni na kushindwa kulimudu kulikopelekea kusombwa na kusababisha vifo vya Wanafunzi nane wenye umri wa miaka kati ya mitatu na kumi na tatu.


Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Mshatakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo ya Wilaya ya Arusha haina mamlaka ya kusikiliza shauri lake ambapo Hakimu Mkazi Mfawidhi Sheila Manento aliahirisha kesi hadi April 30 2024 itakapokuja kutajwa tena.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii