Japan yaitaka Iran 'kujizuia' baada ya kuishambulia Israel

Waziri wa mambo ya nje wa Japan amezungumza kwa simu na mwenzake wa Iran siku ya Jumanne kuitaka nchi yake "kujizuia" ili kuepusha kuongezeka kwa mvutano, kulingana na ripoti ya mazungumzo yao iliyowasilishwa na Tokyo. Haya ni mazungumzo ya kwanza ya moja kwa moja kati ya wakuu wa diplomasia wa nchi hizo mbili tangu mashambulizi ya Iran wikendi hii dhidi ya Israel, ambayo imeahidi kujibu.

Japan ina "wasiwasi mkubwa" na mashambulizi haya ya Irani, ambayo "yanazidi kuzorotesha hali ya sasa katika Mashariki ya Kati", ametangaza mkuu wa diplomasia ya Japan, Yoko Kamikawa, kwa mwenzake wa Iran, Hossein Amir Abdollahian leo Jumanne. Bi. Kamikawa "amehimiza sana Iran kujizuia" ili kuzuia "kuongezeka zaidi kwa mvutano" katika Mashariki ya Kati, ambayo tayari imetikiswa na vita huko Gaza.


Bi. Kamikawa pia ameitaka Iran siku ya Jumanne kuhakikisha usalama wa urambazaji katika maji ya eneo hilo, wakati Tehran ilikamata meli ya makontena, MSC-Aries, katika Ghuba siku ya Jumamosi, ikishutumiwa "kuhusishwa" na Israeli, na kwamba waasi wa Houthi kutoka Yemen, wakiungwa mkono na Iran, wamekuwa wakishambulia meli za wafanyabiashara katika Bahari Nyekundu kwa miezi kadhaa.


Siku ya Jumatatu Mkuu wa majeshi ya Israel Herzi Halevi aliapa kuchukua hatua za kulipiza kisasi dhidi ya Iran baada ya shambulizi lake la mwishoni mwa wiki. Iran ilirusha zaidi ya makombora 300 na droni kuelekea Israel Jumapili usiku.
Baraza la vita la Israel lilifanya kikao kujadili hatua za kuichukulia Iran baada ya shambulizi lake la makombora na ndege zisizo na rubani.


Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliongoza kikao cha baraza la vita la serikali yake jana usiku ambacho kilidumu kwa saa tatu na kujadili hatua zinazoweza kuchukuliwa kujibu shambulizi hilo la Iran. Kwa mujibu wa kituo cha utangazaji cha Channel 12 cha nchini humo, hatua zilizojadiliwa na baraza hilo la mawaziri la vita zilianzia kwa zile ndogo hadi zile kali zaidi. Kiliripoti kuwa Israel inalenga kuweka usawa kati ya kusababisha uharibifu nchini Iran lakini sio kuzusha vita vya kikanda. Mshirika mkuu wa Israel, Marekani, ilisema haifahamu mipango yoyote.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii