Karim Wade akana uria wake wa Ufaransa ili kugombea Urais wa Senegal

Karim Wade, mtoto wa kiume wa aliyekuwa rais wa Senegal na pia kiongozi wa kisiasa mwenye nguvu nchini humo, amekana uraia wa Ufaransa ili kuweza kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu mwezi ujao.

Wade amesema Jumatano kupitia ukurasa wake wa X kwamba waziri wa mambo ya ndani wa Ufarasa amedhibitisha hatua yake.

Uraia wake pacha wa Senegal na Ufaransa umezua gumzo kubwa, kwa kuwa katiba ya Senegal inasema kwamba mtu anaweza kuwania urais pale anapokuwa raia kamili wa Senegal.

Tangazo la Wade limekuja siku chache tu kabla ya tarehe ya mwisho ya kutangazwa kwa orodha ya wagombea, ikiwa imebaki wiki chache kabla ya uchaguzi huo kufanyika mwishoni mwa Februari.

Thierno Allassane ambaye pia ni mmoja wa wagombea wa urais ametoa wito kwa Baraza la Katiba kufuta ugombeaji wa Wade.

Wade anaonekana kuwa mmoja wa wagombea wenye nguvu, na ni mwanachama wa chama cha Demokratik, ambacho kilikuwa cha baba yake Aboulaye Wade, alipokuwa rais kati ya 2000 na 2012.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii