Msiwafunge Biashara, wapeni elimu ya kodi – Meya Kagera

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera, Gypson Godson amepiga marufuku watoza ushuru ndani ya Manispaa hiyo kufunga maduka ya wafanyabiashara na badala yake wajikite kuwapa elimu, ili waweze kulipa Kodi kwa hiyari kama ilivyo azima ya Mhe Rais Dkt, Samia SuluhuHassan.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha Baraza la Madiwani Manispaa hiyo wakati wa kupitisha bajeti katika mwaka wa fedha 2024/2025 Godson amesema elimu iendelee kutolewa kwa Wananchi na Wafanyabiashara kwa ujumla hata kwa kutumia vyombo vya Habari juu ya namna ya kulipa na kukusanya Kodi.

Amesema, Halmashauri hiyo iwafuate wafanya Biashara wote wanaodaiwa na Halmashauri wazungumze nao na watakao kaidi kulipa wafikishwe Mahakamani kama ilivyo kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, Afisa Tawala Wilaya ya Bukoba, Ajesy Katumwa akitoa salamu za Serikali kwenye Baraza hilo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya Bukoba, Erasto Sima ameitaka Halmashari hiyo kuendelea kutoa elimu ya Mapato, ili Wananchi wazidi kupata uelewa wa kulipa kodi kuliko kutumia mabavu.

Awali akisoma taarifa ya mapendekezo ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025, Kaimu Mkurugenzi, Helleni Rocky amesema jumla bilioni 32.6 zimetengwa kwa ajiri ya shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Amevitaja vipaumbele vya maendeleo hayo kuwa ni pamoja na uchumi wa Manispaa hiyo, ujenzi wa soko la dagaa kastam, ujenzi wa maduka eneo la kishenge, ukusanayaji wa mapato na kuweka mikakati ya kutambua na kuongeza vyanzo vipya vya mapato.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii