Watu 26 Wauawa Kwenye Mapigano Mapya Sudan Kusini

MAPIGANO yanayoendelea baina ya makundi tofauti magharibi mwa Sudan Kusini yamesababisha vifo vya angalau watu 26, walisema maafisa wa serikali mnamo Jumanne.

Hayo yalijiri huku rais na makamu wa rais wa taifa hilo wakiyarai makundi hayo kusitisha mapigano hayo ya kikabila.

Zaidi ya watu 150 wameuawa tangu wiki iliyopita, kwenye mapigano tofauti yanayowahusisha vijana kutoka jimbo la Warrap, dhidi ya wenzao kutoka majimbo jirani ya Bahr El Ghazel na Abyei.

Eneo la Abyei huwa linasimamiwa kwa pamoja na Sudan Kusini na Sudan kwa sababu ni eneo la mpakani.

Mapigano hayo hayaonekani kuwa na uhusiano wowote, ijapokuwa yanahusishwa na udhibiti wa ardhi na rasilmali asilia.

Mwanaharakati mmoja alisema kuwa anahofia kwamba kuna misukumo ya kisiasa kwenye mapigano hayo.

Sudan Kusini imekuwa katika hali ya amani tangu 2018, baada ya kutiwa saini kwa muafaka uliomaliza vita vilivyokuwa vimedumu kwa miaka mitano.

Mapigano hayo yalisababisha vifo vya maelfu ya watu huku wengine wakiachwa bila makao.

Licha ya kukamilika kwa mapigano hayo, ghasia baina ya jamii tofauti zimekuwa zikitokea mara kwa mara.

Kulingana na taarifa zilizotolewa na serikali, Rais Salva Kiir alikutana na Makamu wa Rais wa Kwanza Riek Machar, ambapo walitoa wito wa pamoja kwa makundi hayo “kumaliza mapigano ambayo yamekuwa yakiendelea katika baadhi ya sehemu nchini humo”.

Vikosi vya viongozi hao wawili vilikabiliana vikali kweyue vita vilivyodumu kati ya 2013 na 2018.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii