Kenya na Umoja wa Ulaya zasaini mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi

Mkataba huo, umetiwa saini jijini Nairobi, mbele ya rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von Der Leyen na rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi.


Mkataba huo unaeleza kuwa Kenya, itafungua soko lake kwa bidhaa kutoka Ulaya hatua kwa hatua.


 “Hatua hii ni tangazo kwa dunia kuwa Kenya iko tayari kuzalisha bidhaa zenye viwango vya juu kwenda kwenye  soko la Ulaya, ” amesema rais Ruto na kuongeza kuwa Kenya itasafirisha bidhaa zilizokamilika na sio malighafi.


Naye Ursula amesema, hatua hiyo inaimarisha zaidi ushirikiano kati ya Kenya na Ulaya.


“Umoja wa Ulaya, unathamini sana ushirikiano huu. Soko la Ulaya litafunguliwa kwa bidhaa kutoka Kenya,” amesema Ursula akiongeza kuwa mkataba huo uko wazi kwa nchi nyingine za kikanda.


Baada ya kutiwa saini, watalaam kutoka Kenya na Umoja wa Ulaya watakutana kila baada ya miaka mitano kuuthathmini mkataba huo.


Kwa mujibu wa mkataba huo, bidhaa zinazotoka Kenya kwenda kwenye soko la nchi za Umoja wa Ulaya, hazitatozwa kodi.


Miongoni mwa bidhaa ambazo Kenya inatarajiwa kuuza kwenye soko la Ulaya ni pamoja na maua, chai, kahawa, nyama na ngozi, mbogamboga na matunda  miongoni mwa bidhaa nyingine, huku Ulaya ikiingiza bidhaa za viwandani kama dawa na kemikali.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii