Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky siku ya Jumamosi, Aprili 19, ameishtumu Urusi kwa kukiuka usitishaji vita ambao Rais wa Urusi Vladimir Putin alikuwa ametangaza tu kwa ajili ya Pasaka na kwamba Ukraine imeahidi kuheshimu, katika kile ambacho kitakuwa ni mapumziko muhimu zaidi katika mapigano katika miaka mitatu ya mzozo. Kwa rais wa Urusi, tangazo hili linaweza kumuwezesha kupata udhibiti na kuweka kasi kwa mpango wake.
"Ikiwa Urusi iko tayari kujitolea kweli, Ukraine itafanya vivyo hivyo," rais wa Ukraine ameandika kwenye mtandao wa X baada ya tangazo la Kremlin, akiongeza kwamba amependekeza "kurefusha usitishaji vita zaidi ya Aprili 20." Hata hivyo, Jumamosi mchana, Volodymyr Zelensky alihakikisha kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba "mashambulizi ya Urusi yalikuwa yanaendelea katika maeneo kadhaa ya vita," wakati tahadhari ya ulinzi wa anga ilisikika huko Kyiv. "Taarifa za Putin kuhusu Pasaka hazikusikika katika mikoa ya Kursk na Belgorod," ameandika pia.
Volodymyr Zelensky ameripoti kwenye ukurasa wake wa Facebook mapema Jumapili kwamba mashambulizi ya makombora, mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yameendelea usiku kucha. "Kwa ujumla, asubuhi ya Pasaka, tunaweza kusema kwamba jeshi la Urusi linajaribu kuunda taswira ya jumla ya kusitisha mapigano, huku yakiendelea na majaribio ya pekee katika baadhi ya maeneo kuendeleza na kuisababishia Ukraine hasara," rais ameandika, akinukuu ripoti ya Kamanda Mkuu wa Jeshi la Ukraine Oleksandr Syrsky.
Kati ya 12 jioni saa za ndani na usiku wa manane, ripoti imebainisha "milipuko 387 na mashambulizi 19 ya vikosi vya Urusi" pamoja na matumizi ya makumi ya ndege zisizo na rubani. Tangu usiku wa manane, "tayari kumekuwa na kesi 59 za milipuko ya mabomu na mashambulio matano ya vitengo vya jeshi la Urusi." "Mapigano yanaendelea na mashambulizi ya Urusi yanaendelea," amesema mkuu wa jeshi la Ukraine, Oleksandr Prokudin, siku ya Jumamosi jioni. Katika baadhi ya maeneo ya mapigano, mizinga ya Urusi inaendelea kusikika, licha ya ahadi ya kiongozi wa Urusi kusalia kimya. Ndege zisizo na rubani za Urusi zinatumika. "
"Putin ametoka tu kutoa matamshi kuhusu nia yake ya kukubali kusitishwa kwa mapigano. "Tunajua kwamba maneno yake si ya kuaminika na tutachunguza vitendo, sio maneno," ameonya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Andriy Sybiga. Wanajeshi wa Ukraine pia wameonyesha kutokuwa na imani kubwa na Warusi.
Kwa kutangaza ghafla usitishaji vita wakati wa sherehe za Pasaka, Vladimir Putin kwa mara nyingine tena amedhihirisha uwezo wake wa kufika pale ambapo hatarajiwi sana. Ingawa amesema kuwa makubaliano hayo yaliamuliwa na mazingatio ya kibinadamu, kwa kuzingatia umuhimu wa Kanisa katika muundo wa mamlaka ya Urusi, pia inatuma ishara kali kwa raia.
Lakini juu ya yote, rais wa Urusi anajibu wakosoaji wake - Washington na Brussels - ambao wanamtuhumu kwa kujaribu kupata muda kabla ya kutekeleza makubaliano ya siku 30 yaliyoombwa na Ukraine na Marekani.
Kwa usitishaji huu wa mapigano, ambao unatarajiwa kumalizika usiku wa Jumapili 20 kuamkia Jumatatu 21 Aprili, rais wa Urusi anatoa nafasi kwa Kyiv. Moscow inasema jinsi Kyiv inavyoheshimu makubaliano haya itatuwezesha kuamua kupitia azimio lake la kweli kujadili suluhisho la amani na Moscow.
Kwa hakika hii ni mara ya kwanza tangu mzozo huo uanze zaidi ya miaka mitatu iliyopita kwa Urusi kuamuru usitishaji huo wa mapigano.Usitishaji huu vita unahusu sehemu kubwa ya maeneo ya vita na ni wa upande mmoja. Hata hivyo, rais wa Urusi aliweka wazi kwamba vikosi vyake vya jeshi vitajibu ukiukaji wowote wa usitishaji mapigano, pamoja na aina yoyote ya uchochezi wa adui yake.