Uchaguzi umefanyika baada ya wiki kadhaa za ghasia na maandamano, na katika mji mkuu wa Antananarivo wafuatiliaji wanasema uchaguzi umefanyika kwa amani lakini ni idadi ndogo ya wapiga kura walojitokeza.
Upinzani ulitoa taarifa baada ya uchaguzi siku ya Alhamisi, inayosema kwamba idadi ya wapiga kura ilikua ndogo kabisa katika historia ya nchi hiyo, ikitaja takwimu za awali zilizotolewa na wafuatiliaji.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, CENI, inasema haina takwimu rasmi bado na hivyo haitotowa maoni yeyote kwa wakati huu.
Wapiga kura walionekana kwenye vituo vya kura katika maeneo yanayomunga mkono Rais Andry Rajoelina huku vituo kwenye mitaa ya upinzani vilikua kwa sehemu kubwa vitupu.
Vituo vilifungwa saa kumi na moja na matokeo ya awali yanatarajiwa kuanza kutolewa usiku.
Maafisa wa uchaguzi wanasema takwimu za awali za idadi ya wapiga kura walojitokeza maeneo ya chama tawala ilifikia asili mia 30 na ilikua kati ya asili mia 15 hadi 20 katika maeneo ya upinzani, hiyo ikiashiria kwamba watu huwenda wamechukizwa na uchaguzi huo.