Ahmed Ally afichua ujio wa Benchikha

Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amefichua siri iliyomvuta Kocha Mkuu wa klabu hiyo kwa sasa Abdelhak Benchikha ambaye tayari ameshawasili jijini Dar es salaam.

Kocha huyo anayetamba kwa kutwaa Ubingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kuifunga Young Africans msimu uliopita na CAF Super Cup kwa kuisasambua Al Ahly, amewasili nchini usiku wa kuamkia leo akiwa sambamba na wasaidizi wake Farid Zemiti (Kocha Msaidizi) na Kamal Boudjenane (kocha wa viungo).

Ahmed ally amefichua siri hiyo zikisalia saa kadhaa kabla ya kocha huyo kutambulishwa kwa Mashabiki na Wanachama wa Simba SC katika Mkutano na Maalum wa waandishi wa Habari utakaofanyika leo Jumanne (Novemba 28) jijini Dar es salaam.

Ahmed ametumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kuainisha siri hiyo, huku akiwataja viongozi wa Simba SC kuwa chanzo cha ushawishi ambao ulifanikisha safari ya Benchikha kutoka Algeria hadi Tanzania.

Ahmed Ally ameandika: Kilichomvutia Mwalimu Benchika kujiunga na Simba ni mipango endelevu ya klabu yetu

Benchikha anataka kufanya kazi kwenye taasisi yenye maono mapana na yenye malengo makubwa

Benchikha ameangalia maendeleo yetu ndani ya kipindi cha miaka 6 na kujiridhisha kuwa Simba ni sehemu sahihi kwake.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii