Maisala kwenda jela miaka 20 kisa bangi

Mkazi wa Kisiwa cha Maisome wilayani Sengerema mkoani Mwanza, Maisala Ramadhani (25) ameangua kilio mahakamani baada ya kuhukumiwa jela miaka 20 baada kukiri kosa la kukutwa na dawa za kulenya aina ya bangi nyumbani kwake.

Hukumu hiyo ya kesi ya jinai namba 121/2023, imetolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya wilaya ya Sengerema, Evod Kisoka.

Awali, akisoma maelezo mbele ya Hakimu, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Morice Mtoi amesema mshtakiwa alikamatwa Oktoba 9, 2023, na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa wilaya ya Sengerema, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Titho Mohe.

Mwendesha mashtaka huyo amesema mshtakiwa alikamatwa na askari huyo katika kisiwa cha Maisome kambi ya wavuvi ya Migongo akiwa na Bhangi kilogramu 10 kwenye nyumba yake ya kuishi.

Pamoja na maombi ya mshtakiwa (Maisala) kuomba kupunguziwa adhabu, Mahakama imemhukumu kifungo hicho cha miaka 20 ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo kulingana na madhara yasababishwayo na madawa ya kulevya.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii