Watu 48 wafariki dunia kufuatia kimbunga Otis

Takriban watu 48 wamekufa kufuatia kimbunga Otis kilichopiga pwani ya kusini katika bahari ya Pasifiki nchini Mexico.

Mji wa Acapulco ndio ulioathirika zaidi. Viongozi wa Mexico wamesema idadi ya vifo inaendelea kuongezeka huku familia zikianza kuwazika wapendwa wao.

Shirika la ulinzi wa raia la Mexico limesema watu 43 kati ya waliofariki walikuwa katika mji wa mapumziko wa Acapulco na watano katika mji wa Coyuca de Benitez. Gavana wa jimbo la Guerrero Evelyn Salgado amesema idadi ya watu ambao haijulikani walipo imeongezeka kutoka 10 hadi 36.

Shughuli za uokozi zinaendelea lakini wakazi karibu milioni moja wa Acapulco  bado wanakabiliwa na uhaba wa maji safi, umeme. Mamlaka nchini Mexico imesema karibu nyumba 220,000 zimeharibiwa na kimbunga Otis, na kwamba imeongeza idadi ya wanajeshi eneo hilo hadi kufikia 15,000 ili kuzuia wizi na uporaji.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii