Tuzo ya BBC ya Komla Dumor ya 2022 yazinduliwa

BBC inamtafuta nyota anayechipukia katika uandishi wa habari barani Afrika kwa ajili ya Tuzo ya BBC World News Komla Dumor, ambayo sasa ni mwaka wake wa saba.

Waandishi wa habari kutoka kote barani Afrika wanaalikwa kutuma maombi ya kuwania tuzo hiyo, ambayo inalenga kuibua na kukuza vipaji vipya kutoka barani humo.

Mshindi atatumia miezi mitatu katika makao makuu ya BBC mjini London, kupata ujuzi na uzoefu.

Maombi yatafungwa tarehe 16 Februari 2022 saa 23:59 GMT.

Tuzo hiyo ilianzishwa kwa ajili ya kumuenzi Komla Dumor, mtangazaji wa kipekee kutoka Ghana na mtangazaji wa BBC World News, aliyefariki ghafla akiwa na umri wa miaka 41 mwaka 2014.

Mjane wa Dumor, Kwansema Dumor alimwambia mshindi wa awali, Victoria Rubadiri, alisema "anajivunia'' mazuri aliyoyafanya mume wake katika BBC, na pia alisema familia yake "inatoa shukrani kwa BBC kwa kumkumbuka" kupitia tuzo hiyo.

BBC inawahimiza wanahabari kote barani Afrika kutuma maombi kwa ajili ya tuzo hiyo, ambayo inalenga kukuza na kusherehekea vipaji bora vya uandishi wa habari wanaoishi na kufanya kazi katika bara la Afrika.

Pamoja na kupata mafunzo, atakayefaulu atapata fursa ya kusafiri hadi nchi barani Afrika kuripoti habari ambayo wameifanyia utafiti, ripoti hiyo ikitangazwa kwa hadhira ya kimataifa ya BBC.

Akijulikana kwa kusimamia uandishi wa habari thabiti na mahiri na kwa kujitolea kwake kuripoti hadithi za Kiafrika kwa ukamilifu na uhalisia, Dumor alileta matokeo makubwa kwa Afrika na kwingineko duniani.

BBC imejitolea kuendeleza urithi wake kupitia tuzo hiyo kwa kuwawezesha wanahabari kutoka Afrika kueleza hadithi za Kiafrika asilia na zenye za kipekee ili kufikia hadhira ya kimataifa.

Kwa sababu ya janga la virusi vua corona, Rubadiri hakuweza kufanya mafunzo yake mnamo 2020, kwa hivyo iliahirishwa hadi 2021.

Wakati akiwa kazini alisafiri hadi Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ili kuripoti kuhusu programu iliyotengenezwa ili kuboresha usalama wa usafiri.

Rubadiri alikabidhiwa tuzo hiyo na Mkurugenzi Mkuu wa BBC Tim Davie.

"Zaidi ya heshima kubwa ya kuinua kumbukumbu ya marehemu Komla Dumor, na uzito wa BBC kutambua kazi yangu kama mwandishi wa habari, nimeona ukuaji ndani yangu katika miezi mitatu iliyopita niliyokaa London," alisema.

"Mafunzo yaliinua ujuzi wangu hadi ngazi nyingine. Fursa hii ilinipa mtazamo wa bara la soko la habari na kunifungua akili kwa njia mpya za kusimulia hadithi ya Kiafrika."

Liliane Landor, mkurugenzi wa BBC World Service, alisema: "Nimefurahi kwamba Tuzo ya BBC World News Komla Dumor imerejea kwa mwaka wake wa saba.

"Washindi waliotangulia wameonesha mfano wa kujitolea kwa Komla katika kusimulia hadithi za Afrika kwa kina, elimu na maarifa. Tunafuraha kupata na kumkaribisha mshindi wa mwaka huu na kuona urithi wa uandishi wa habari wa Komla ukiendelea."

Dumor alikuwa mtangazaji wa Focus on Africa, kipindi cha kwanza kabisa cha BBC cha habari za kila siku za televisheni kwa Kiingereza kwa watazamaji wa Kiafrika, kilichotangazwa kwenye BBC World News. Pia alikuwa mmoja wa watangazaji wakuu wa kitengo cha asubuhi cha BBC World News' Ulaya.

Alijiunga na BBC mwaka wa 2007 baada ya muongo mmoja wa uandishi wa habari nchini Ghana ambako alishinda tuzo ya Mwanahabari Bora wa Mwaka wa Ghana.

Kati ya 2007 na 2009 alikuwa mwenyeji wa Network Africa kwa BBC World Service, kabla ya kujiunga na kipindi cha The World Today.

Mwaka wa 2009 Dumor alikua mtangazaji wa kwanza wa kipindi cha habari za biashara za Kiafrika kwenye BBC World News, Africa Business Report. Alisafiri kote barani Afrika, akikutana na wafanyabiashara wakuu barani Afrika na kuripoti juu ya mitindo ya kisasa ya biashara kote barani.

Mwaka 2013 Dumor alishiriki katika orodha ya jarida la New African la Waafrika 100 wenye ushawishi mkubwa zaidi.



Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii