BAADHI ya wanahabari waliofika katika mahakama ya Milimani mnamo Ijumaa, Julai 21, 2023 kunasa matukio wakati wa kesi dhidi ya Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, wamepata wakati mgumu baada ya kunyanyaswa na maafisa wa polisi.
Wanahabari hao walikua wamefika kuangazia uamuzi wa mahakama kumuachilia kwa dhamana Bw Owino ila walipata wakati mgumu baada ya maafisa wa polisi kuwazuia kuingia ndani ya mahakama.
Hakimu alimwachilia Bw Owino kwa dhamana ya pesa taslimu Sh100,000 katika kesi ya uasi inayohusiana na maandamano dhidi ya serikali ya inayoendeshwa na Muungano wa Azimio La Umoja.
Baada ya kuachiliwa kwake, wafuasi wa mbunge huyo waliokua wamefika mahakamani walianza kusherehekea wakitoka nje ya mahakama na punde mzozo ulizuka.
Maafisa wa polisi wa kupambana na ghasia waliokuwa wakimngoja mbunge huyo nje ya mahakama, walianza kuwashambulia wanahabari waliokuwa nje tayari kunasa picha hizo.
Katika video iliyonaswa, maafisa hao wa polisi wanaonekana wakimsukuma mpigapicha wa gazeti la Standard Bw Collins Kweyu huku wakimshambulia.
Baadaye Kweyu anaonekana akiwa ameanguka kwenye ngazi baada ya kusukumwa na polisi huku akiwa ameshikilia kamera yake.
Amekiri kushambuliwa na maafisa wa polisi wa kupambana na ghasia akisema kuwa waliendelea kumsukuma licha ya kujitambulisha kuwa mwandishi wa habari.
Alisema kuwa alipata jeraha kwenye goti lake la kushoto na bado anahisi maumivu kwa sasa.
“Ndiyo. Walinisukuma. Goti langu la kushoto lilijeruhiwa na ninahisi maumivu hivi sasa. Nilijitambulisha kuwa ni mwanahabari lakini hawakuwa tayari kunisikia. Kwa sasa bado nahisi maumivu na itanilazimu nitafute matibabu hospitalini,” Bw Kweyu akasema.