Mtumiaji wa intaneti raia wa Morocco amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kumkosoa mfalme kwenye mtandao wa Facebook juu ya hatua ya Morocco kuboresha uhusiano na Israel.
Said Boukioud, mwenye umri wa miaka 48, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela siku ya Jumatatu kwa kuchapisha ujumbe kwenye Facebook ambao unakosoa uhusiano na Israel kwa njia ambayo inaweza kutafsiriwa kama kumkosoa mfalme, wakili wake El Hassan Essouni alisema, akiongeza kuwa amekata rufaa.
Kulingana na katiba ya nchi, masuala ya nje yako chini ya mamlaka ya mfalme Mohamed wa sita.
Morocco na Israel zilianzisha tena uhusiano wao mwezi Disemba mwaka wa 2020 kama sehemu ya makubaliano yanayoungwa mkono na Marekani.
Hukumu ya mahakama ya Cassablanca “ni kali na haieleweki”, wakili huyo alisema.
Ameongeza kuwa licha ya mteja wake kupinga uhusiano na Israel, hakuwa na nia ya kumkashifu mfalme kwa kufanya hivyo.