Straika Mpya Yanga, Mayele Mtupu Kutoka Cameroon

UONGOZI wa Yanga, umekamilisha taratibu za usajili wa mshambuliaji Emmanuel Mahop Dikongue kutoka Cameroon ambaye sifa zake zinafafana na Mkongomani, Fiston Mayele.

Yanga inamsajili mshambuliaji huyo ilia kuchukua nafasi ya Mayele ambaye hakuwepo katika utambulisho wa juzi kwenye Tamasha la Kilele cha Wiki ya Wananchi lililofanyika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Imeelezwa kuwa, Yanga imemuuza Mayele kwenda Pyramids FC ya Misri ikinunua mkataba wa mwaka mmoja kwa dau la Sh bilioni 2.1, huku mshambuliaji huyo akichukua mshahara wa Sh milioni 80 kwa mwezi.

Mmoja wa Viongozi wa Kamati ya Mashindano na Usajili ya Yanga, ameliambia Spoti Xtra kuwa, wamefikia makubaliano mazuri ya kumsajili mshambuliaji huyo kwa mkataba wa miaka miwili.

Kiongozi huyo alisema, wamefiikia hatua ya kumsajiili kutokana na sifa alizonazo mshambuliaji huyo kufanana na Mayele katika kufunga na kutengeneza mabao.

Alizitaja sifa hizo ni uwezo wa kukokota mpira huku akipiga mashuti kwa kutumia miguu yote miwili, nguvu, maarifa na wepesi wake akiwa ndani ya 18 kwa wapinzani.

“Muda wowote huenda tukamtambulisha Emmanuel kuwa mbadala wa Mayele ambaye yeye hatakuwa sehemu ya kikosi chetu katika msimu ujao baada ya kukubali kumuuza.

“Mshambuliaji huyo ana sifa zote za sisi kumsajili ambazo ni uwezo mkubwa wa kufunga mabao, nguvu, maarifa na wepesi wake ndani ya 18 ya goli la wapinzani.

“Pia uwezo wake wa kukokota mipira huku akipiga mashuti kwa kutumia miguu yote miwili kama alivyokuwa kwa Mayele, hivyo hatujutii usajili wake,” alisema kiongozi huyo.

Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, juzi alisema: “Bado hatujafunga usajili licha ya kutangaza wachezaji wetu wapya tutakaowatumia msimu ujao katika Kilele cha Wiki ya Wananchi.”

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii