Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi huenda hakufika hata katika shule ya upili kinyume na vyeti alivyonavyo vinavyosema, mpelelezi ameambia mahakama.
Derrick Juma ambaye ni mpelelezi kutoka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) katika kesi ambapo mbunge huyo anatuhumiwa kughushi vyeti vyake vya masomo, aliambia mahakama kuwa Sudi aliacha shule akiwa darasa la saba.
"Vyeti vya Oscar Sudi vya shule ya upili na chuo kikuu ni bandia. Mbunge huyo aliacha shule katika darasa la saba na huenda hakusonga mbele kwenda sekondari," Juma amenukuliwa na chapisho la the Standard.
Tathmini ya mchunguzi huyo kuhusu ushahidi ilimfanya ahitimishe kuwa mbunge huyo alighushi cheti chake cha KCSE na cheti cha diploma ambacho alitumia alipotafuta kibali cha kuwania kiti chake cha ubunge 2013. Juma alisema vyeti hivyo vilikuwa na jina lisilo sahihi la shule ya upili, nambari za watahiniwa wengine, nambari ya msimbo wa shule tofauti na sahihi zilizoghushiwa kwenye cheti cha kumaliza shule.