Mamlaka nchini Uhispania zimefahamisha kuwa zimefanikiwa kuwaokoa wasaka hifadhi 86 karibu na visiwa vya Canary ambao walikuwa kwenye mashua ndogo inayoaminika ilitokea nchini Senegal ikielekea barani Ulaya.
Hayo yanajiri wakati shirika la misaada la Walking Borders linasema watu wasiopungua 300 waliosafiri kwa kutumia boti tatu kutoka Senegal kuelekea Uhispania wamepotea baharini na hadi sasa hakuna mawasiliano yoyote yaliyofanyika na vyombo hivyo.
Kikosi cha Huduma ya Uokoaji wa Baharini ya Uhispania kimesema hakikuweza kuthibitisha ikiwa mashua iliyookolewa ilikuwa moja ya tatu zilizoripotiwa kutoweka.
Njia ya uhamiaji kupitia Bahari ya Atlantiki ndiyo hatari zaidi duniani na takwimu zinaonesha kuwa karibu watu 800 wamekufa au kupotea baharini katika nusu ya kwanza ya mwaka huu.