MMOJA wa wandani wa karibu wa mhubiri wa Kanisa la Good News International Paul Mackenzie ameaga dunia huku wengine wawili wakilazwa hospitalini wakiwa katika hali mahututi.
Upande wa mashtaka umeambia mahakama kwamba Joseph Juma Buyuka ameaga dunia hospitalini Malindi alipokuwa amelazwa ili kupokea matibabu.
“Tunashuku kwamba mshukiwa amefariki kutokana na athari ya kususia chakula. Ingawa hivyo, tutasubiri matokeo ya ripoti ya upasuaji wa maiti,” amesema wakili Jami Yamina.
Buyuka alikuwa miongoni mwa washukiwa 30 wandani wa Mackenzie waliopelekwa katika gereza la Malindi GK baada ya kususia mlo katika seli za Shanzu.
Buyuka alipelekwa katika hospitali ya Malindi hali yake kizuizini iliposambaratika. Alifariki wakati akipokea matibabu.