Ajabu Maiti Ikifufuka Ecuador

WAOMBOLEZAJI katika mazishi ya mwanamke  nchini Ecuador, walipigwa na butwaa baada ya  kugundua kuwa marehemu bado alikuwa hai licha ya kutangazwa kufariki na madaktari.

Bella Montoya, 76, alitangazwa kufariki wiki iliyopita baada ya kuugua Kiharusi (stroke) na baadaye kufa.

Hata hivyo, saa tano, usiku wa kuamkia Ijumaa,Juni 9, 2023 familia ikijiandaa kubadilisha nguo zake kabla ya mazishi, ilipatwa na mshangao walipompata akipumua.

Kwa sasa Bi Montoya amerejeshwa hospitalini kwa uangalizi zaidi, huku Wizara ya Afya ya Ecuador ikiunda kamati kuchunguza tukio hilo la ajabu.

Ecuador ni nchi iliyoko Magharibi mwa Pwani ya Amerika Kusini.

Kupitia taarifa, wizara hiyo ilisema kwamba mwanamke huyo alipatwa na mshtuko wa moyo na baadaye kukosa kujibu walipojaribu kumfufua huku daktari wa zamu akithibitisha kifo chake.

Mwanawe, Gilber Rodolfo Balberán Montoya, alinukuliwa na vyombo vya habari vya Ecuador akisema kwamba mama yake “alilazwa mwendo wa 09:00, na saa sita mchana daktari alimpa habari ya tanzia.”

Bi Montoya aliwekwa kwenye jeneza kwa saa chache ili kuipa familia muda kumuaga.

Video iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii ilionyesha Bi Montoya akiwa amelazwa kwenye jeneza lililo wazi, akipumua kwa nguvu huku watu kadhaa wakisongea kumtazama.

Wahudumu wa afya kisha wanaonekana wakiwasili na kumtazama Bi Montoya kabla ya kumsogeza kwenye machela na kuingia kwenye ambulensi na kuondoka.

Kwa sasa yuko katika chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali ileile ambapo madaktari walitangaza kifo chake.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii