Vita vyapamba moto Khartoum

Mashambulizi ya anga na mizinga yameongezeka kwa kasi katika mji mkuu wa Sudan siku ya Jumanne asubuhi, wakaazi wa mji huo walisema, wakati jeshi likijaribu kulinda kambi muhimu kutoka kwa wapinzani wa kijeshi ambao wamekuwa wakipambana nao kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Mashambulizi ya anga, milipuko na mapigano yaliweza kusikika kusini mwa mji wa Khartoum, na kulikuwa na mashambulizi makali ya makombora katika maeneo mbali mbali ya mto Nile yanayopakana na miji ya Bahri na Omdurman, mashuhuda walisema.

Mapigano kati ya jeshi na vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) yamesababisha machafuko katika maeneo mengine ya Sudan, hususani katika eneo la Darfur Magharibi, lakini mapigano zaidi yako katika jiji la Khartoum.

Mzozo huo umesababisha mgogoro wa kibinadamu ambao unatishia ukosefu wa utulivu katika eneo hilo, ambapo zaidi ya watu 700,000 wamekoseshwa makazi nchini Sudan na wengine takriban 200,000 kulazimika kukimbilia nchi jirani.

Wale ambao wamebaki katika mji mkuu wanahangaika kujikimu kimaisha kadiri upatikanaji wa chakula unavyopungua, huduma za afya zikiporomoka na uasi kuenea.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii