Mlinzi mmoja nchini Uganda aliwafungia nje wafanyakazi 50 wa serikali kwa madai ya kutolipwa malimbikizo ya mshahara wake.
Karim Kanku, 67, anasemekana kudai serikali takriban KSh1.8 milioni za malimbikizo ya mshahara katika muda wa miezi tisa iliyopita.
Kanku anasema amevumilia nyakati ngumu, ikiwa ni pamoja na familia yake kukosa chakula, kulipa kodi ya nyumba na karo ya shule. Wafanyikazi walioripoti kazini Jumatatu asubuhi walishtuka kupata jengo nzima limefungwa.
Tukio hilo liliwathiri wageni waliofika katika afisi hizo za serikali huku baadhi ya wafanyakazi wakitumia fursa hiyo kuenda nyumbani. Bado haijabainika wazi namna Kanku alipata funguo hizo, lakini duru zinasema kwamba kwa sababu amefanya kazi katika Manispaa ya Njeru kwa zaidi ya miaka 30, alikuwa akiaminiwa na wakubwa wake.
“Kama watanisimamisha kazi kwa sababu ya kufunga ofisi, wafanye hivyo; lakini wanapaswa kulipa pesa ninazowadai kwa miezi tisa iliyopita. Nimejaribu kuwa mvumilivu wakati huu wote kana kwamba sina majukumu nyumbani,” alisema.
Kanku anasema amekuwa akifanya kazi zamu ya mchana na usiku, mara nyingi bila likizo na kwamba aliwahi kuomba kuongezewa mlinzi mwingine ambaye wanaweza kusaidiana lakini ombi lake lilidharauliwa. Kando na kuwa mlinzi, Kanku anasema pia alijumuika na wafanyikazi wengine saba wa kusaidia kudhibiti taka katika manispaa hiyo.
Huku akidai malimbikizo ya mshahara ya miezi miwili kwa kudhibiti taka, wenzake wanaripotiwa kudai malimbikizo ya mishahara ya miezi mitatu. Mwenyekiti wa Kitengo cha Kati cha Njeru, Michael Odeba, ambaye afisi yake pia ilikuwa imefungwa, aliwapongeza Kanku na wakusanyaji taka, akiongeza kuwa changamoto hiyo ilisababishwa na serikali Kuu.