Ikiwa zimepita siku kadhaa tangu litokee tukio la kijana mmoja jijini Arusha kumuua mama yake mzazi kwa tamaa ya mali, limeibuka tukio lingine la kinyama mkoani Kilimanjaro katika Manispaa ya Moshi.
Inaelezwa kuwa binti mmoja aliyejulikana kwa jina la Wendy amemuua mama yake mzazi (Mama Ipepu) ambaye ni nesi mstaafu wa Hospital ya KCMC kisha kuuzika mwili wake jirani na nyumbani pasipo majirani na wanandugu kufahamu.
Baada ya kupata taarifa na kuzifanyia kazi, Jeshi la Polisi liliufukua mwili huo leo jana Jumapili Januari 9, 2022 katika Kata ya Rau baada ya kumhoji binti huyo kwa zaidi ya wiki mbili sasa kisha kukiri kumchinja mama yake kwa panga na kumfukia nyumbani hapo.
Ni takribani mwaka sasa ndugu na majirani walipokuwa wakimuulizia mama huyo walipatiwa majibu na binti huyo kuwa amesafiri kwa matibabu nje ya nchi.
Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Juma Raibu amelaani vikali tabia ya vijana kuendekeza tamaa na kukosa uvumilivu wa utafutaji mali kisha wanaishia kufanya matendo ya kinyama.
"Kiukweli hili ni tukio la kutisha, nitoe pole kwa familia ndugu na majirani wote mliofika hapa, nimepata huzuni sana kuona jinsi gani ya tamaa mali imetufikisha hapa, nalaani na ninatoa wito kwa vijana wenzangu wote nchini kuacha kupaparikia mali na starehe, mwisho wake tunageuka kuwa wanyama kiasi hiki.
“Yaani unamuua mama mzazi? Hivi unakuwa huogopi laana na adhabu ya Mola? Nalipongeza jeshi letu la Polisi kwa hatua hii, nawatia moyo mwendelee na kazi hii njema ya kufichua na kudhibiti wahalifu wa namna hii na wanaoshirikiana nao."
Madaktari wameanza kufanyia uchunguzi wa postmortem mwili huo kwa ajili ya hatua zinazofuata.
MALI ZA BABA
Inadaiwa kuwa binti huyo aliona mama yake ni kikwazo cha kurithi mali hasa ardhi iliyoachwa na baba yake, Dk Pima Ebreck.
Kamanda wa Polisi Moa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alipoulizwa alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kusema uchunguzi unaendelea