Agnes Nandutu, alikamatwa Jumanne, Aprili 18, alipojisalimisha kwa polisi ili kuhojiwa kuhusiana na sakata ya kutoweka kwa mabati ya Karamoja. R
Waziri Nandutu, alifikishwa mbele ya Mahakama ya Kupambana na Rushwa siku ya Jumatano Aprili 19, na kushtakiwa kwa kuhusika na mali inayoshukiwa. Hata hivyo, Nandutu alikanusha mashtaka hayo huku mwendesha mashtaka wa serikali, David Bisamuyu akiambia mahakama kwamba uchunguzi wa polisi kuhusu kesi yake ulikuwa umekamilika.
Japo Nandutu alishiklia kuwa hana hatia, Bisamuyu alisema alikuwa na maagizo kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka kumpeleka katika Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi hiyo. Nandutu, ambaye ni mwanahabari wa zamani wa runinga, anashukiwa kuwa miongoni mwa viongozi wakuu serkalini waliogawana mabati 12,000. Inaripotiwa kwamba takriban mawaziri 20 na wabunge 35 kote nchini Uganda wamehusishwa na kashfa hiyo akiwemo Makamu wa Rais, Waziri Mkuu Robinah Nabbanja, spika wa Bunge Anita Miongoni na Waziri wa Fedha, Matia Kasaija.
Akiwahutubia waandishi wa habari muda mfupi baada ya Mahakama ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Kololo, Kampala kumfikisha katika Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi yake, Nandutu alikosoa namna kesi yake ilivyoendeshwa. "Ninakubali kuwa nimebatizwa kwa moto. Niko imara. Hata hivyo, kwa nini nipelekwe katika Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi wakati mahakama ya chini (Kupambana na Rushwa) ndiyo yenye mamlaka ya kushughulikia kesi hii?" alimaka waziri huyo.