Baba ajiua yeye na wanae kisa ugumu wa maisha

Imeelezwa Mzee Amani Madumba aliyekuwa akiishi Kata ya Ruaha Mbuyuni wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro aliyefariki dunia yeye pamoja na watoto wake watatu usiku wa kuamkia leo Mei 5, 2023 kwa kuteketea kwa moto, kwamba yeye ndiye aliyeichoma nyumba hiyo kisa ugumu wa maisha.

Ndugu wa marehemu aitwaye Rajab Madumba, amesema ndugu yao huyo wakati wa uhai wake alikuwa akilalamika kwamba endapo yeye akifariki basi watoto wake watabaki wakiteseka na pengine ndiyo sababu ya kuamua kuiteketeza familia yake hiyo.

Kwa upande wake mdogo wa marehemu aitwaye Salum Madumba amesema, "Kaka angu alizaa na mwanamke wake lakini baadae nilipata taarifa kuwa waliachana kwa sababu ya marehemu kuwa na hali ngumu ya kimaisha, hivyo ndivyo ambapo walitengana na kila mtu kuishi kivyake lakin kukawa na utaratibu wa kuwa watoto wanaweza kumtembelea baba yao ambaye alikuwa akijishughulisha na ushonaji wa maturubai,". 

Aidha Salum ameongeza, "Ila siku tatu nyuma alikuwa akisema kwamba kama nikifa hivi karibuni naomba michango yangu wapewe watoto wangu lakini mpaka kufikia jana aliwaita wanae watatu nyumbani kwake  na ndipo usiku wa manane moto ulipozuka nyumbani hapo na kupoteza maisha,".


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii