Watu 56 wauawa Sudan katika mapigano ya siku mbili

Takriban watu 56 wameuawa nchini Sudan  na wengine zaidi ya 400 wamejeruhiwa katika siku mbili za  mapigano makali yaliyozuka kati ya jeshi la nchi hiyo na kundi la wanamgambo la RSF linalopigania udhibiti wa taifa hilo lililokumbwa na machafuko tangu 2021.


Wakazi walikwepa milio ya risasi katika mji mkuu, Khartoum, wakati vikosi hasimu vikipigania ikulu ya rais, TV ya serikali na makao makuu ya jeshi. Wananchi wa Sudan wamesema mzozo huu unakumbusha  enzi za utawala wa Rais wao wa  zamani  Omar al-Bashir .Kampuni ya pili ya mawasiliano ya Sudan ya MTN imefunga mtandao kufuatia maagizo kutoka kwa mamlaka, maafisa wake waliambia Reuters.

Mzozo huo ulioanza siku ya Jumamosi unatokana na mvutano kuhusu pendekezo la mpito kwa utawala wa kiraia ambao umekuwa ukionekana kwa miezi ya hivi karibuni kati ya kiongozi wa kijeshi wa Taifa la Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na Kiongozi wa RSF Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo.

Nchi na taasisi mbalimbali duniani zimelaani ghasia hizo. China imesema inasikitishwa sana na maendeleo ya hali ya Sudan na kutoa wito kwa pande zote mbili za mzozo kusitisha mapigano haraka iwezekanavyo ili kuepusha kuongezeka kwa hali hiyo .

Umoja wa Afrika umetoa wito wa kusitishwa kwa mapigano haraka katika taarifa yake.
"Leo wakati mambo yameshindwa kudhibitiwa na kusababisha vurugu za kutumia silaha kutumika kama njia ya kusuluhisha mizozo ya kisiasa, Rais wa Tume ya Umoja wa Afrika anatoa wito kwa pande zote, vikosi vya jeshi na RSF kukomesha mara moja uharibifu wa nchi, hofu ya watu na umwagaji damu wa watu wasio na hatia katika siku 10 za mwisho  za mwezi mtukufu wa Ramadhan".Taarifa ya OAU imeeleza.

Wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanasema  chimbuko la mzozo wa sasa unarejea katika kipindi cha Rais Omar al-Bashir, ambaye alitawala nchi hiyo kwa takriban miaka 30 kabla ya kupinduliwa kupitia maandamano makubwa mwaka 2019. Kumekuwa na maandamano ya mara kwa mara ya kuunga mkono demokrasia mjini Khartoum tangu mapinduzi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii