Mamaye Mwanachuo Aliyeuawa Alaani Unyama Wa Polisi
MAMA yake mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Maseno aliyeuawa Jumatatu wakati wa maandamano ya Upinzani, amesikitika na kusema hakuwahi kuwazia kuwa mwanawe angefariki kabla hajahudhuria sherehe ya kufuzu kwake mwakani.
Eveline Miruka, 44 akiwa amesononeka na kudondokwa na machozi, ni mamaye William Mayenga, mwanafunzi wa mwaka wa tatu aliyeuawa wakati wa maandamano ya Azimio la Umoja, Jumatatu.
Kile kinachomuumiza sana Bi Miruka ni kwamba mwanawe pekee ndiye aliuawa wakati wa maandamano hayo.
Ni Jumatatu ya wiki jana ambapo alizungumza na mwanawe kisha akamtumia pesa za matumizi huku akimwaahidi kwamba angemwongezea nyingine baadaye.
Kumbe hiyo ndiyo ilikuwa mara yake ya mwisho kuzungumza na Bw Mayenga, kifungua mimba wake.
“Nilisikitika na kushangazwa na taarifa nilizopata. Mwanzo walinidanganya kuwa mwanangu alikuwa hai ila nilipofika hospitalini nilipata alikuwa amefariki,” akasema Bi Miruka.
Alisema kuwa alitarajia mwanawe awe mwalimu kama yeye na baba yake. Hata hivyo, sasa hilo halitawezekana kwa sababu ya uhai wake kuondolewa kupitia risasi iliyofyatuliwa na polisi.
“Mwanangu alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu na alistahili kufuzu mwaka ujao. Sikujua kuwa kufuzu huku ni kuchukua mwili wa mwanangu mbele ya lango la shule,” akasema Bi Miruka akiwa na jamaa zake katika Chumba cha Kuhifadhia Maiti cha Coptic ambapo mwili wa mwanawe upo.
Alishikilia kwamba mwanawe hana sifa yoyote ya uhalifu na anataka haki itendeke kuhusu mauaji yake.
“Badala ya polisi kuwalinda watoto wetu, wanawaua. Mtoto wangu hakuwa jangili auawe kama wale wanaosumbua Bonde la Ufa. Alifanya nini? Yeye si Mhalifu. Ninataka haki itendeke kwa mwanangu,” akasema Bi Miruka.
Bi Miruka ni mwalimu wa Kiingereza na Sayansi katika Shule ya Msingi ya Emaruba. Babake, Joash Bangi Mayenga, naye ni mwalimu wa Hisabati katika Shule ya Upili ya Birongo, Kaunti ya Nyamira.
Babaye, 54 ambaye alifika mochari hiyo akiendeshwa kwa gari kutoka Keroka na nduguye Joel, hakuamini macho yake kwamba ni mwanawe aliyekuwa ameuawa kinyama.
“Siamini mwanangu amekufa kutokana na jeraha baya kama hilo. Sikuwazia kuwa siku moja kutatokea hali ambapo nitamzika mwanangu,” akasema.
Alisikitika kwamba aliwekeza katikati masomo ya mwanawe na malipo yake sasa ni polisi kumuua kinyama.Bw William na marehemu walizungumza mara ya mwisho Ijumaa na alikuwa atimu umri wa miaka 22 hapo Mei.
Polisi walidai walitekeleza mauaji hayo kwa sababu wanafunzi hao walivamia kituo chao wakati wa maandamano hayo yaliyokuwa yameagizwa na Kinara wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga.
Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii