Mama atupa kichanga kisa ugumu wa maisha

Prisca Lameck mwenye umri wa miaka 28 mkazi wa Nyakato jijini Mwanza anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani humo kwa tuhuma za kumtupa mtoto wake mwenye umri wa miezi mitatu akidai kuwa ugumu wa Maisha ndiyo umemsababisha kufanya hivyo.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa amesema baada ya mwanamke huyo kutupa kichanga chake hicho eneo la Buswelu wilayani Ilemela wasamaria wema waliweza kumuokota akiwa hai huku mama huyo akishikiliwa na jeshi la polisi 

"Baada ya mahojiano ya kina mtuhumiwa huyo alikiri kutupa kichanga hicho baada ya kumuhoji akadai hali ya maisha ni ngumu lakini sisi tunasema hiyo haiwezi kuwa sababu ya kusababisha ukazaa mtoto na kumtelekeza sababu bado kuna taasisi nyingi unaweza kupeleka shida zako wakakusaidia kutunza mtoto" amesema kamanda Mutafungwa 
Katika tukio lingine Kamanda Mutafungwa amesema watu wawili wanashikiliwa kwa tuhuma za kuiba injini ya boti moja aina ya YAMAHA iliyokuwa inatumika kwenye mradi wa ujenzi wa daraja la JPM eneo la kigongo busisi 

"Kupitia doria na oparesheni zetu kali tumeweza kuikamata na watuhumiwa amabo walikuwa wameiba walikuwa wameipakia kwenye bajaji watuhumiwa wawili tunawashikilia na injini boti yenyewe tunayo na watu wa mradi wamefika na kuthibitisha kuwa hiyo injini ilikuwa inatumika kwenye mradi watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kuwa umekamilika"

Kamanda Mutafungwa amesema jeshi la polisi linaendelea kutoa elimu ya usalama barabarani hususani katika kipindi hiki cha wiki ya nenda kwa usalama na kusema madereva wanaokiuka sheria za barabarani wanaendelea kuchukuliwa hatua za kisheria huku akiwatahadharisha na madereva wengine kuzingatia sheria za usalama barabarani.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii