JESHI la Polisi Mkoa wa Morogoro, limesema wafugaji ambao walikimbia makazi yao kutokana na mapigano yaliyoibuka kati yao na wakulima katika Kijiji cha Itete wilayani Malinyi wamerejea baada ya hali kuwa shwari kutokana na polisi kuimarisha doria katika eneo hilo.
Katika mapigano hayo yaliyotokea Desemba 17, 2021 kwenye skimu ya umwagiliaji, mkulima Abdul Magwila (34) alifariki dunia na wengine wanne kujeruhiwa huku kaya 18 zikichomwa moto na kusababisha baadhi ya wafugaji kukimbia makazi yao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Musilim amesema hali ya utulivu imerejea na wafugaji ambao walikimbia makazi yao kutokana na vurugu hizo wamesharejea baada Jeshi la Polisi kuimeimarisha doria.
Amesema baada ya kutokea kwa tukio hilo, Polisi ilianza uchunguzi kwa kundi la wafugaji walioingiza mifugo ndani ya skimu ya umwagiliaji huku waliohusika kuchoma nyumba za kaya 18 wakiendelea kusakwa.
Naye, Mwenyekiti wa wafugaji wilaya ya Malinyi, Mtalimbo George amesema baada ya kutokea kwa vurugu, makazi ya wafugaji yaliyo karibu na skimu ya umwagiliaji Itete yalivamiwa na kundi la wananchi na kuchomwa moto huku akidai kuwa baadhi ya mali zikiwamo mazao na mifugo ziliporwa.
“Baada ya mkulima mmoja kupoteza maisha na wengine wanne kujeruhiwa, wananchi wamelipiza kisasi kwa kuchoma nyumba za wafugaji moto na zile ambao zimenusurika, kuku na mpunga ulikuwa ukiibwa na kundi la wananchi,” amesema Mtalimbo.