Watu 67 wamekufa leo baada ya ndege yenye uwezo wa kubeba abiria 72 kuanguka kwenye korongo wakati ikitua katika uwanja mpya wa ndege uliofunguliwa kwenye mji wa Pokhara nchini Nepal.
Kwa mujibu wa afisa mkuu katika wilaya ya Kaski ,Tek Bahadur K.C. waokoaji wanaendelea kupekua eneo la ajali na wanatarajia kupata miili zaidi katika ajali hiyo iliyotokea karibu na Mto Seti takriban maili moja kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Pokhara.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Nepal imesema katika taarifa yake kwamba ndege hiyo yenye injini mbili aina ya ATR 72 inayoendeshwa na shirika la ndege la Yeti la Nepal ilikuwa imebeba abiria 68, wakiwemo raia 15 wa kigeni, na wafanyakazi wanne.
Haijabainika mara moja kilichosababisha ndege hiyo kuanguka. Waziri Mkuu wa Nepal Pushpa Kamal Dahal, aliyekwenda haraka kwenye eneo la mkasa baada yaajali hiyo, amewataka wahudumu wa usalama na wananchi kwa ujumla kusaidia katika juhudi za okoaji.