Watu 8 wafariki katika shambulizi la Al-Shabaab nchini Somalia

Polisi wa Somalia wamesema kwamba watu wanane wameuawa katika shambulio la bomu kando ya barabara, huko Buloburde, mji ulipo katika wilaya ya Hiran ambapo vikosi vya serikali na wanamgambo wa ukoo wamekuwa wakipambana na waasi Al-Shabaab tangu mwaka jana. Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi wa eneo hilo Abdullahi Mohamud, Al-Shabaab imedai kuhusika na shambulizi hilo ambalo mshambuliaji alilipua gari lililokuwa na vilipuzi karibu na jengo la utawala. Kando na shambulizi hilo polisi walisema bomu jengine lililotegwa ndani ya gari lililipuliwa katika eneo la Jalalaqsi, mji mwingine kwenye wilaya ya Hiran, lakini ni mshambuliaji pekee aliyekufa. Kwa miaka 15 wanamgambo wa Al- Shabaab wamekuwa wakiendesha uasi wa umwagaji damu dhidi ya serikali dhaifu mjini Mogadishu inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa, wakifanya mashambulizi nchini Somalia na nchi jirani. Katika miezi ya hivi karibuni, jeshi na makundi ya wapiganaji wa koo nchini humo wamechukua udhibiti wa maeneo mengi katika operesheni iliyoungwa mkono kwa mashambulizi ya anga ya Marekani na kikosi cha Umoja wa Afrika.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii