Polisi wa nchini Brazil imeisambaratisha kambi ya waandamanaji nje ya makao makuu ya jeshi la nchi hiyo siku moja baada ya wafuasi wa rais wa zamani Jair Bolsonaro kuyavamia majengo ya utawala kwenye mji mkuu Brazilia.
Operesheni hiyo imefanyika baada ya Mahakama ya Juu ya Brazil kutoa amri ya kuondolewa kambi zote za waandamanaji ikiwemo iliyowekwa mbele ya makao makuu ya jeshi kufuatia hujuma za siku ya Jumapili. Polisi pia imewakamata zaidi ya waandamanaji 1,500 wanaohusishwa na uvamizi huo kwenye majengo ya Bunge, Mahakama ya Juu na ofisi rasmi ya rais wa nchi hiyo.Miongoni mwa hatua nyingine ni uamuzi wa Mahakama ya Juu wa kumwondoa madarakani kwa muda wa siku 90 gavana wa jimbo la Brazilia Ibaneis Rocha anayetuhumiwa kutochukua hatua za kuimarisha usalama licha ya ishara zote za tahadhari zilizoonekana.