Jeshi la Urusi limedai kufanya mashambulizi ya angani katika kambi ya kijeshi inayotumiwa na majeshi ya Ukraine kama hatua ya kulipiza kisasi kwa vifo vya wanajeshi wa Urusi waliouwawa kutokana na shambulizi la roketi wiki iliyopita.
Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema makombora yake yamezilenga kambi mbili za muda za kijeshi zilizokuwa makao ya wanajeshi 1,300 huko Kramatorsk mashariki mwa Donetsk.
Msemaji wa wizara hiyo Igor Konashenkov amesema mashambulizi hayo ni ya kulipiza kisasi cha lile shambulizi la Ukraine mjini Makiivka lililowauwa wanajeshi 89 wa Urusi.
"Katika siku moja iliyopita, idara ya ujasusi ya Urusi imegundua na kuthibitisha kupitia njia kadhaa huru, kambi za kijeshi za Ukraine mjini Kramatorsk. Kulikuwa na zaidi ya wanajeshi 700 katika chumba nambari 28 na zaidi ya wanajeshi 600 katika chumba nambari 47.
Zaidi ya wanajeshi 600 wa Ukraine wameuwawa kutokana na shambulizi hili kubwa la roketi."Maafisa wa Ukraine lakini wamekanusha mauaji yoyote yaliyotokana na mashambulizi hayo.