Ukraine Yapokea Silaha Za Kujikinga Na Makombora, Russia Imetengua Ndege Isiyo Na Rubani Ya Ukraine

Rais wa Ukraine Volodymr Zelenskyy amepongeza msaada wa silaha kutoka Marekani, unaojumuisha magari yenye uwezo wa kurusha makombora ya kuharibu vifaru vya kivita.

Zelenskyy amesema kwamba msaada huo uliotolewa na Marekani wa mabilioni ya dola ndio unaohitajika kwa Ukraine ambayo inaendelea kupambana na wanajeshi wa Russia.

Maafisa wamesema kwamba haijulikani iwapo Moscow itaheshimu tangazo la kusitisha vita kwa muda wa saa 36 kwa ajili ya kusherehekea krismasi kwa waumini wa dhehebu la Orthodox.

Msaada wa hivi punde wa kijeshi kwa Ukraine ndio mkubwa zaidi kuwahi kutolewa.

Katika hotuba ambayo imepeperushwa mara kadhaa na vyombo vya habari nchini Ukraine, rais Zelenskyy ameutaja msaada wa Marekani kuwa wenye nguvu sana.

Ukraine imesema kwamba tangazo la kusitisha vita lililotolewa na Russia kwa ajili ya krismasi ya Orthodox, limekiukwa na baadhi ya wanajeshi wake wanaoendelea kupigana wakati vita hivyo vinaingia mwezi wa 11.

Russia imesema imeangusha ndege isiyokuwa na rubani ya kurusha makombora ya Ukraine

Gavana wa mji wa Sevastopol, ambaye aliyeteuliwa na Russia baada ya kuudhibithi mji huo kutoka kwa Ukraine, ameandika ujumbe wa Telegram akisema kwamba wanajeshi wa Russia wameangusha ndege isiyokuwa na rubani, iliyokuwa inalenga kuushambulia mji huo.

Mikhail Razvozhael, ameashiria kwamba ndege hiyo imetumwa na Ukraine kutekeleza mashambulizi wakati wa sherehe za krismasi kwa waumini wa kanisa la Orthodox.

Russia iliinyakua Crimea kutoka kwa Ukraine mnamo mwaka 2014.

Ukraine imesema kwamba ina lengo la kurejesha sehemu zote ambazo zimechukuliwa na Russia zikiwemo zilizochukuliwa kabla ya uvamizi wa sasa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii