NDUGU WAWILI WAHUKUMIWA KWENDA JELA MIAKA 10 KWA KUJARIBU KUMUUA MAMA YAO MDOGO KWA KUMPIGA NA NYUNDO KICHWANI

Mahakama ya hakimu mkazi Njombe imewahukumia kutumikia kifungo cha miaka 10 gerezani Focus lutengano na Aizack Lutengano baada ya kuwakuta na hatia ya kujaribu kumua mama yao mdogo Rehema Ngimbudzi mkazi wa kijiji cha mtwango wilayani Njombe kwa kumpiga na nyundo kichwani.

Akisoma hukumu hiyo katika kikao cha mashauri ya mauaji ambacho kimefanyika Mahakama ya mwanzo Makambako Hakimu mkazi mkuu mwenye mamlaka ya ziada Liadi Chamshama amesema washtakiwa hao walitenda kosa hilo Septemba 21, 2016.

Licha ya adhabu ya kutumikia miaka kumi jela, wametakiwa kumlipa Mama yao mdogo Rehema Ngimbudzi kila mmoja fedha kiasi cha shilingi milioni Tano.

Aidha Hakimu huyo wakati akisoma maelezo ya washtakiwa hao aliamuru mdhamini wa mshtakiwa namba moja bwana Christopher Joseph Salingwa kulipa faini ya shilingi milioni 4 au kwenda jela mwaka mmoja kwa kosa la kushindwa kumfikisha mshtakiwa mahakamani,ambapo shahidi huyo amelipa faini hiyo.

Awali mawakili wa washtakiwa hao, Happy Ilomo wakili wa mshtakiwa namba mbili Focus Lutengano na wakili Brighton kagua wakili wa mshtakiwa namba moja Aizack Lutengano waliomba Mahakama hiyo kuwapunguzia adhabu kwani wanategemewa na familia na ni mara yao ya kwanza kutenda kosa hilo.

Lakini hata hivyo wakili wa serikali Andrew Mandwa alimtaka hakimu kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa wengine.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii