Jeshi la Somalia lawashinda wanamgambo walioivamia hoteli

Polisi nchini Somalia imesema operesheni dhidi ya wanamgambo wa al-Shabaab waliokuwa wameingia katika hoteli ya mjini Mogadishu imemalizika na magaidi wote sita waliokuwa wakitafutwa wameuawa. Msemaji wa polisi hiyo, Sadik Dodishe amesema mmoja wa maafisa wa usalama waliohusika katika operesheni hiyo pia alipoteza maisha.

Dodishe amearifu kuwa watu 60 waliokuwa wamenaswa katika hoteli hiyo yenye ulinzi mkali ya Villa Rose wameondolewa wakiwa salama salimini. Hata hivyo, wakaazi wawili wa mji wa Mogadishu waliozungumza na shirika la habari la Associated Press wamesema jamaa zao, wote raia wa kawaida waliuawa katika uvamizi huo. Kupitia kituo chake cha redio, kundi la al-Shabaab lilidai kuhusika na shambulizi hilo kwenye hoteli inayopendelewa na maafisa wa serikali.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii