Mnunuzi wa madini auwa

Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya linamshikilia Ezekia Luhweshe (31) mchimbaji na mnunuzi wa madini, wilayani Chunya, mkoani Mbeya kwa tuhuma za mauaji ya wakala wa maegesho ya magari aitwaye William Mgaya (58) mkazi wa Mama John jijini Mbeya.


RPC Mbeya, ACP Benjamin Kuzaga, amesema tukio hilo limetokea Novemba 26, zilipo ofisi za TARURA katika jengo la TAFISA lililopo Kata ya Ruanda jijini humo, ambapo imeelezwa marehemu akiwa na mwenzake walimkamata Ezekiel, baada ya ku-scan namba yake ya gari T.772 DVY Toyota Hilux na kugundua kuwa gari hilo lina deni la sh.7,500.


Mtuhumiwa alitakiwa kulipa deni hilo lakini alihitaji kuona hilo deni linatokana na maegesho gani hivyo kulazimika kuongozana naye hadi zilipo ofisi za TARURA kwa ajili kuangalia kwenye mfumo ili kupata taarifa za deni hilo. 


Mtuhumiwa alionyeshwa taarifa za deni hilo na kuridhika kuahidi kulipa deni hilo lakini wakala Mgaya alimtaka kulipa deni hilo papo hapo kutokana na deni hilo kuwa la muda mrefu ndipo yalitokea majibizano kati ya marehemu na mtuhumiwa hali iliyopelekea mtuhumiwa kutoa silaha yake Pistol na kufyatua  risasi moja uelekeo alipokuwa Mgaya  na kumpiga sehemu ya kifuani upande wa kulia na kusababisha kifo chake muda mfupi baada ya kufikishwa Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa matibabu.

 

Mtuhumiwa pamoja na Silaha Pistol aina ya Tisasi yenye namba T.0620-19J0037 ya mtuhumiwa ikiwa na risasi tisa ndani ya magazine anashikiliwa na Jeshi la Polisi.


Kamanda Kuzaga ACP ametoa rai kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake watoe taarifa za malalamiko yao au kitendo chochote wanachofanyiwa kinyume cha sheria au taratibu zilizopo kwa viongozi wa mamlaka husika kwa ajili ya ufuatiliaji na hatua zaidi za kisheria.

 

Aidha Kamanda Kuzaga ametoa wito kwa wale wote wanaomiliki silaha kuzingatia masharti ya umilikishwaji wa silaha hizo pamoja na kuhakikisha silaha hizo wanazitumia kulingana na hitaji au mahitaji ya msingi waliyoombea silaha hizo na sio kutishia ama kuua watu jambo ambalo ni kinyume cha sheria za nchi na masharti ya umiliki wa silaha.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii