Mshukiwa mkuu wa kisa cha mtoto kung’olewa macho awekwa rumande
Bi Pacificah Nyakerario, 60, alikamatwa na maafisa
wa upelelezi Jumatatu usiku katika maficho yake jijini Nairobi, na
kusafirishwa kurudi nyumbani na makachero hao.

Alikuwa ametoroka Kisii mnamo Desemba 14, baada ya
Sagini kushambuliwa katika kisa ambapo macho yake yaling’olewa kikatili
katika kijiji cha Ikuruma, Kaunti Ndogo ya Marani.
Sagini aligunduliwa akiwa ametelekezwa katika shamba la mahindi lililo karibu na kwao.
Alikimbizwa hospitalini kupata matibabu.
Mshukiwa huyo alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Bi Christine Ogweno Jumanne asubuhi lakini hakujibu chochote.
Hakimu Ogweno alisema mwanamke huyo atasalia rumande
hadi Ijumaa wiki hii ambapo atarudishwa tena kortini kesi yake
itakapotajwa.
Wakati huo huo, nusura kizaazaa kizuke nje ya
mahakama hiyo, baadhi ya wanawake waliokuwa wamekusanyika hapo
kufuatilia kesi, kudai kuwa amechafua jina la watu watokao Marani.
Hata hivyo, polisi walifanikiwa kutuliza mvutano wao.
Akiwa kizimbani, Bi Nyakerario alilia kwa uchungu upande wa mashtaka ulipokuwa ukimsomea mashtaka yake.
“Utarudishwa rumande katika Kituo cha Polisi cha
Rioma hadi Ijumaa wiki hii utakapofikishwa hapa kwa ajili ya kutajwa kwa
kesi yako,” Hakimu alisema huku akimtaka mkuu wa kituo cha polisi
kumhakikishia usalama wake.
Bi Nyakerario, ambaye ni shangazi wa Sagini,
alifikishwa mahakamani siku moja baada ya mshukiwa wa kwanza ambaye ni
mwanawe – Alex Maina Ochogo,28, kufikishwa mbele ya hakimu huyo pia.
Sagini na dadake mkubwa Shantel Ongaga, 7, watahamishwa hadi kwenye hifadhi salama jijini Nairobi.
Gavana wa Kisii Simba Arati, juzi alisema kwamba
alipokea simu kutoka kwa Waziri wa Jinsia Aisha Jumwa akimjulisha kuhusu
dhamira ya serikali ya kuhakikisha watoto hao wanaendelea kupata
matibabu na utunzaji.
“Jioni hii nilipokea simu kutoka kwa Waziri Jumwa na
akakubaliana nami kwamba watoto hao wawili wapelekwe kwenye hifadhi
nzuri na salama Nairobi. Nimeagiza gari la kaunti lipatikane ili
kuwapeleka watoto hao huko,” Bw Arati alisema.
Hatua hii ilijiri saa chache baada ya Mwakilishi wa
Wanawake wa Kisii, Bi Dorice Aburi, mwenzake wa Busia Catherine Omanyo
na seneta mteule Gloria Orwoba kumtembelea Bi Jumwa katika afisi yake
jijini Nairobi ambapo walijadili hali ya Sagini.
Katika mkutano huo, Bi Aburi alibainisha pia kuwa
walijadiliana kuhusu jinsi anavyoweza kufanya kazi na serikali ya
kitaifa ili kulinda na kukuza ustawi wa Wakenya.
Aliongeza kuwa mipango ya kuwa na kituo cha kuwaokoa
wanaonyanyaswa, kilichojengwa mjini Kisii imeanza kwa kasi na hivi
karibuni kitaanza kufanya kazi.
Jana Jumanne, maafisa kutoka idara ya kuwalinda
watoto walimchukua dadake Sagini kutoka kijijini Ikuruma huku mipango ya
kuwasafirisha wawili hao Nairobi ikikaribia kutamatika.
Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii