Iran imesema imemnyonga mtuhumiwa mwengine aliyetiwa hatiani kutokana na vurugu kwenye maandamano yanayopinga utawala wa Kiislamu wa nchi hiyo. Vyombo vya habari nchini Iran vinasema Majidreza Rahnavard alitiwa hatiani kwa kuwauwa maafisa wawili wa usalama.
Pia alikutikana na kosa la kutangaza "vita dhidi ya Mungu", ambalo adhabu yake ni kifo kwa sheria za Iran. Rahnavard amenyongwa chini ya mwezi mmoja tangu aliposhukiwa kufanya mauaji hayo kwa kutumia kisu. Makundi ya haki za binaadamu yanasema watuhumiwa wengine kadhaa waliotiwa nguvuni na vyombo vya dola wanakabiliwa na hatima kama hiyo.
Iran ilitekeleza hukumu ya kwanza ya aina hiyo kwa watuhumiwa wanaohusika na maandamano wiki iliyopita, baada ya kumnyonga Mohsen Shekari mwenye umri wa miaka 23. Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya walikutana jana Jumatatu kujadili hukumu hiyo, wakitazamiwa kutangaza vikwazo zaidi dhidi ya utawala wa Iran.